Zosima, yule mzee mtawa alikuwa ameenda jangwani wakati mmoja wa Mfungo Mkuu. Kwa siku ishirini, alikuwa akitembea jangwani ng’amboni mwa Yordani. Ghafla, akatazama na kukiona kivuli cha mtu aliyeonekana mkavu wa nyama iliyokuwa uchi na nywele nyeupe kama theluji, alionekana akitoroka machoni pa Zosima. Mzee Zosima alimkimbiza kwa muda mpaka ambapo mfano huu wa mtu ulisimama mahali pa kijito na kuita: “Padre Zosima, nisamehe kwa ajili ya Bwana. Siwezi kukugeukia, mimi ni mwanamke na sina nguo”.
Zosima alimrushia vazi lake la juu liitwalo rasso, akajifuka na kumgeukia. Mzee Zosima alishangaa sana kusikia mwanamke asiyemuona tena akimuita kwa jina lake halisi. Zosima alimsihi sana kwa muda mrefu amwambie yeye ni nani mpaka wakati ambao ulikuwa mgumu kulitupilia mbali ombi lake na hivyo, ikabidi afunguke na kumwambia yote kuhusu maisha yake ila jina lake hakumwambia, alimuonya asimwambie yeyote kumhusu mpaka atakapokufa.
Alikuwa mzaliwa wa Misri na alikuwa jangwani sasa kwa miaka arubaini na saba. Akiwa na umri wa miaka kumi na miwili, alijitoza katika uzinzi (ukahaba) na kudumu katika maishi hayo ya anasa kwa miaka kumi na saba.
Huku akiwashwa na mapenzi yake ya uzinzi, siku moja akaliona meli lililokuwa liking’oa nanga kuelekea Yerusalemu kwa ibada ya Usujudu wa Msalaba Mtakatifu na Mhuishaji wa Kristo. Hakuwa na hela za kulipia nauli na kwa matamanio yake ya kwenda kuliko na umati alikojua kuwa biashara yake itanoga, alipeana mwili wake kwa wahudumu wa meli na hivyo kutimiza azma yake ya kufika mji Mkuu Mtakatifu wa Yerusalemu. Baada ya hii miaka mingi ya kuishi katika anasa hata za ulevi, mwili wake ulikuwa umejawa na joto la uzinzi na hakuwa anafanya tena kama biashara bali kama njia ya kutosheleza joto la mwili wake tu.
Walipofika, alianza kutafuta na kulala na wanaume hata wengine wakiwa ni watu wa kuheshimika katika kanisa na jamii lakini kwa urembo wake, walijipata kuanguka katika majaribu yake. Siku ya kuusujudia Msalaba ilipofika, alifuatana na umati ulioelekea katika kanisa la Kaburi Takatifu kwa Usujudu wa Msalaba Mtakatifu. Aliwafuata na kujaribu kuingia nao kanisani humo lakini nguvu zisizoonekana zilimzuia mlangoni asiweze kuingia hata baada ya kujaribu mara yasiyopungua tatu ya kung’ang’ana kwingi.
Kwa hofu nyingi, alitazama na kuiona Ikoni takatifu ya Mama wa Mungu. Kwa machozi mengi, alianza kuwaza jinsi huyu Mzazi-Mungu alivyoweza kuyashinda ya ulimwengu kwa unyenyekevu na wema mwingi maishani mwake; huku akijitazama yeye mwenyewe na maisha yake ya anasa, alimsihi Mzazi-Mungu kumpa nafasi aingie kanisani humo angalau ausujudie Msalaba Mtakatifu na Mhuishaji wa Mwanawe na Mungu wetu Yesu Kristo kabla ya kuondoka na kwenda atakakomwelekeza.
Kwa unyenyekevu mwingi baada ya kukubaliwa kuingia, alijiunga na waumini wengine waliokuwa tayari wamo kanisani. Alitubu makosa yake na kuusujudia Msalaba kabla ya kutoka mlangoni palipokuwa na ile Ikoni, alimshukuru Mzazi-Mungu na hapo akasikia sauti: “Utakapovuka Yordani, utapata amani iliyo ya kweli”. Huku akitoka kuelekea alikoelekezwa, mtu asiyejua alimpa hela tatu na akazitumia kununua mikate mitatu na kuondoka.
Alifika Yordani jioni ya siku hiyo. Asubuhi ya siku iliyofuata, alipokea Mwili na Damu ya Kristo katika Monasteri ya Mtakatifu Yohana na hapo baadaye akauvuka mto.
Wakati alipokuwa akivuka mto wa Yordani, alikuwa amebakisha mikate miwili na nusu. Baada ya muda, mikate hiyo ikawa migumu sana na alikuwa akikata kidogo tu ya kujiweka hai. Kwa miaka kadhaa, aliishi tu kwa hiyo mikate na baadaye akaanza kuishi kwa mimea na matunda tu mikate ilipoisha.
Kwa hiyo miaka arubaini na saba akiwa jangwani, majaribu mengi ya kurudia mambo ya kale yalimwandama kama mazimwi yaogofyayo lakini, kwa machozi mengi na kuomba, yalitupiliwa mbali kwa neema.
Wakati mmoja, Zosima alimuona akiwa ameinuliwa juu huku akiomba bila kushikiliwa na chochote kionekanacho. Alimsihi Zosima amletee Ushirika wa Mwili na Damu ya Kristo mwaka uliofuata katika ufuo wa Yordani na akamhakikishia kuwa atakuja kupokea.
Zosima alibeba Vipaji Vitakatifu mwaka uliofuata na kwendwa alikoagizwa. Alimuona yule mwanamke akivuka mto kama nchi kavu baada ya kufanya ishara ya Msalaba juu ya maji. Baada ya kupokea Ushirika Mtakatifu, Zosima alimsikia akisema; “Sasa Bwana umruhusu mtumishi wako aende kwa amani, kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako”. Kisha akamsihi Zosima kurudi tena mwaka uliofuata katika kijito walichokutania mwanzo.
Aliporudi mwaka uliofuata, aliupata mwili wake mahali pale walipokutania mwanzo. Aliyaona maandishi mchangani juu ya mkono wa huyu mwanamke yaliyosoma; “Padre Zosima, uzike hapa mwili wa Maria Mnyenyekevu. Rudisha undongo undongoni. Nililala Aprili 1, jioni ya siku ya Mateso ya Kristo, baada ya kushiriki Fumbo Takatifu. Hapo ndipo Zosima alijua mara ya kwanza jina la huyu mwanamke na kushangaa kwamba alifika kwenye hicho kijito siku hiyo hiyo alipomshirikisha kwa vipaji vitakatifu…
* Sofroni Patriakha wa Yerusalemu wala si Aleksandria, samahani
source
Recent posts
Apolitikio ya Pentekoste
Hebu jiulize
Apolitikio ya Kuzaliwa kwa Kristo (Live class with Nyandarua Youths)